Friday, August 24, 2007

BURIANI AMINA CHIFUPA; VIJANA TUMEKUSIKIA!



Wiki hii taifa la Tanzania hususan jamii ya Vijana lilikumbwa na msiba mzito wa kuondokewa na Mbunge wa Viti Maalum (UV-CCM), Mhe. Amina Chifupa Mpakanjia aliyefariki tarehe 26.06.2007, baada ya kuugua kwa muda mfupi. Kimsingi msiba huu ni pigo kubwa sana kwa wanajamii wote na hasa sisi tulio katika mapambano ya kuwakomboa Vijana.

Mhe. Amina tulifahamiana kwa muda mfupi sana lakini kwa kipindi hicho kifupi, niligundua ni mtu mwenye msimamo usioyumba. Mwezi July, mwaka jana, niliandika makala kwenye gazeti hili juu ya Amina makala iliyokuwa na kichwa: “HONGERA MHE. CHIFUPA; WABUNGE WENGINE VIJANA MPO WAPI?” Baada ya makala hiyo nilipokea simu toka kwa waheshimiwa wabunge na mawaziri mbalimbali akiwemo Marehemu Amina mwenyewe, tulizungumza mengi na kuweza kuonana na tokea hapo, ndipo tulipozidi kuwa na ukaribu ulionifanya niweze kumfahamu Mhe.Amina kwa kiasi fulani.

Kwa kipindi kifupi nilichomfahamu Marehemu Amina, kimsingi nilijifunza mengi, hivyo leo nina ujasiri wa kumuandika na kusema kweli safari yake fupi hapa duniani haikuwa ni ya hasara, Marehemu Amina ameondoka kijasiri, Amekufa kishujaa. Amina amelala lakini bado fikra, mwelekeo, malengo, na kauli zake bado zinaishi na zitaishi milele yote. Ninakumbuka wakati alipokuwa anagombea Ubunge kupitia Jumuiya ya Vijana (UVCCM), jinsi ambavyo alikumbana na vikwazo mbalimbali kutoka kwa watu tofauti, wengine walidiriki hata kumuandika kwenye vyombo vya habari waziwazi wakimbeza na kumkashifu kuwa hafai kuwa mbunge, lakini yeye alisimama kidete na kulinda heshima na hadhi yake na hatimaye alifanikiwa kuvuka vikwazo hivyo na kuwa Mbunge mwenye umri mdogo kuliko wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata baada ya kuingia bungeni, Mhe Amina hakuwa kimya kama wengi walivyodhani, bali alisimama imara na kuonesha wazi nia na wajibu uliompeleka bungeni wa kuwatetea Vijana. Hivyo leo tunasikia Amina amefariki, tunajua wazi kuwa Vijana tumempoteza mwakilishi wetu hodari na aliyekuwa na nia ya kutusaidia.

Uwakilishi wa Mhe. Amina haukuishia kuchangia mijadala kwenye vikao vya Bunge tu, bado tulimsikia na kumuona akifanya shughuli mbalimbali za kijamii, kama kuwatembea vijana na watoto wenye matatizo mbalimbali, kwa hili tuliona jinsi Mhe. Amina alivyokuwa na moyo wa kuwatumikia Vijana na wanajamii wa Kitanzania.

Pamoja na kumkumbuka Mhe. Amina, ni vema sisi kama Vijana na wanajamii tukajiuliza ni kitu gani tumejifunza kutoka kwake, je ni jambo gani tutakalomkumbuka nalo maishani mwetu. Mimi binafsi kama Mwanaharakati na mdau wa masuala ya Vijana, nimejifunza mambo mengi kutoka kwa marehemu Amina na mambo hayo ni chamamoto kubwa kwangu katika wajibu na nafasi yangu ya kuwatumikia Vijana. Ninaomba niwakumbushe vijana na wanajamii mambo machache niliyojifunza kutoka kwa Mpendwa wetu huyu.

Amina alikuwa ni mwanaharakati, mpambanaji na mwakilishi mwenye nia na mikakati mingi na mizuri kwa ajili ya vijana siku za mbeleni. Mapambano ya Amina dhidi ya matatizo ya vijana na hususan suala la matumizi ya dawa za kulevya ni sehemu tu ya vitu ambavyo vilimjengea heshima kubwa kwa jamii na vijana na wote wenye mapenzi mema na maisha ya vijana hapa nchini. Ninakumbuka alisema kuwa yupo tayari kufa kwa ajili ya kuwatetea vijana wanaokabiliwa na matatizo mengi ya ukosefu wa kazi, elimu duni, ukosefu wa maeneo huru ya kufanyia biashara na suala la mmomonyoko wa maadili.

Marehemu Amina alikuwa ni kijana mwenye nia na malengo ya kufika mbali, hii ni pamoja na kusimama kwake kidete akilinda na kutetea nafasi yake kwa wale wote waliokuwa na nia ya kumkwamisha na kumrudisha nyuma, Amina alifahamu umuhimu wa elimu na ndio maana mpaka wakati anafariki licha ya kuwa alikuwa ni Mbunge, bado alikuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Mambo haya na mengine mengi yanamfanya Amina awe kioo kwetu kama Vijana na wanajamii wengine. Ninapenda kuwakumbusha wapendwa kuwa, katika kumuenzi na kumkumbuka Marehemu Amina ni wajibu wetu kusimama katika mstari ule aliosimama na kuutetea siku zote. Kwa waheshimiwa wabunge hususan wabunge vijana, mnapaswa kufahamu kuwa mna wajibu mzito wa kuwatetea vijana wenzenu bungeni na pia katika maeneo mbalimbali mnayoweza kuyafikia. Zaidi kuzidisha mapambano juu ya tatizo la dawa za kulevya ili vita hii ambayo Mhe. Amina aliipigania hadi siku ya umauti wake iweze kushinda na vijana wakombolewe katika hilo.

Kwa wapendwa vijana wenzangu, Mhe. Amina alikuwa ni mtu mwenye ujasiri wa kupigania haki yake na hadhi aliyonayo kijamii, hivyo ni wajibu wetu leo kama Vijana kuhakikisha kuwa na sisi tunatetea na kulinda hadhi yetu kijamii, hadhi hii inapaswa kulindwa hata ikibidi kufa, lakini tusikubali mtu awaye yote atudhalilishe na kutudharau eti kwa kuwa sisi ni vijana. Mhe. Amina alikuwa ni mtu mwenye kutafuta elimu, hivyo ni wajibu na nafasi yetu kama vijana kuhakikisha kuwa na sisi tunaitafuta sana elimu bila kujali kiwango cha elimu tuliyo nayo sasa, tuhakikishe kuwa maadamu tunaishi tunasoma hadi mwisho wa maisha yetu. Mhe. Amina alikuwa ni mtu mwenye kuishi bila makuu licha ya ubunge wake. Hayo ni mambo ambayo sisi kama Vijana tunapaswa kuyaiga toka kwa marehemu Amina na kuyaenzi yale yote aliyoyaacha kwetu.

Wiki hii katika makala yangu, nilipanga kuandika tena juu ya suala la dawa za kulevya hasa ukizingatia kuwa ilikuwa ni wiki ya maadhimisho ya kupiga vita na kudhibiti matumizi ya dawa hizo. Hata hivyo suala la hilo nililiacha baada ya kusikia habari za msiba huu wa kusikitisha wa Mpendwa wetu Amina Chifupa Mpakanjia (Mbunge wa Vijana), sijui kama wengi tunalifahamu hili, lakini ni kuwa Marehemu Amina alikuwa anapigania sana suala la athari za matumizi ya dawa za kulevya kwa Vijana. Kwa neema, Mungu amemchukua Amina siku ya kilele cha kupambana na dawa za kulevya na siku hiyo (26.06.07), Mhe. Rais Jakaya Kikwete alikuwa Mjini Tanga kwenye maadhimisho ya siku hiyo ya kupambana na dawa hizo za kulevya. Hivyo Amina alikuwa ni Mpiganaji wa kweli katika tatizo hili, na hata Mungu anajua.

Mwanaharakati wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, marehemu Steve Biko aliyeuwawa kinyama na makaburu mwaka 1978 akiwa kijana mdogo, alikufa akiwa na falsafa hii, “HERI KUFA UKIWA NA KAULI INAYOISHI; KULIKO KUISHI UKIWA HUNA KAULI!”. Nimeikumbuka falsafa hii baada ya kifo cha Mhe. Amina. Ni kweli kuwa Amina amekufa, Amina amelala na wala hatutakaa tumuone tena katika maisha ya kibinadamu, lakini kauli zake zinaishi na kauli hizi zitaishi hata mwisho wa dunia. Hivyo Mpendwa Amina ninapenda kusema, VIJANA TULIKUPENDA, LAKINI MUNGU ALIKUPENDA ZAIDI, NENDA KAPUMZIKE DADA, LAKINI FAHAMU KUWA SISI KAMA VIJANA NA WANAJAMII TUNAKUMBUKA NA KUENZI MAMBO YOTE MAZURI ULIYOYAACHA!

Msahafu wa Kikristo (Biblia) unassema, “MTU AWAYE YOTE ASIUDHARAU UJANA WAKO, BALI UWE KIELELEZO KWAO WAAMINIO, KATIKA USEMI, KATIKA MWENENDO, KATIKA UPENDO, NA KATIK AIMANI NA USAFI! –2 Timotheo 4:12–13.

Kweli Amina umelinda heshima ya Ujana wako na ndio maana sisi tunasema kuwa, tumejifunza kutoka kwako kuwa, kuishi bila kauli ni mbaya, heri kufa ukiwa na kauli inayoishi. Mwenyezi Mungu aipumzishe Roho yako mahali pema peponi, Upumzike kwa Amani.

Mungu Ibariki Tanzania! Mungu wabariki Vijana wa Tanzania!

Hillary N. Mkony,
Mwanaharakati wa masuala ya Vijana,
S.L.P. 743, Simu: 0754 000 215,
ARUSHA.

No comments: