Friday, August 24, 2007

"MHESHIMIWA KIKWETE; VIJANA WANASEMA HIVI ..........."


Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naomba leo nitumie nafasi na ukurasa huu wa Kona ya Vijana kuzungumza nawe juu ya mambo machache ambayo nimekuwasikia vijana wanayazunguza na kutamani kuyafikisha kwako juu ya serikali yako na namna wanavyokutazama katika nafasi yako juu ya mustakabali wa maisha yao chini ya jua hili. Hivyo ninaomba ufahamu kuwa vijana wengi wana mengi ya kusema nawe kama ilivyo kwa watanzania wengi, tatizo kubwa ni namna ya kufikisha kauli yao hiyo kwako. Hivyo mimi naomba nibebe wajibu huo wa kuwa kipaza sauti cha vijana kwa kufikisha kauli yao kwako.

Awali ya yote napenda kukupa pole kutokana na majukumu mengi ya kuwatumikia watanzania, majukumu uliyokabidhiwa na wananchi kupitia sanduku la kura mnano tarehe 14.12.2005. Mungu akuwezeshe kuyatekeleza kwa faida ya watanzania walioonyesha matumaini na matarajio makubwa juu yako. Kila la kheri.

Mheshimiwa Rais, tarehe 12.08. kila mwaka Tanzania itaungana na mataifa mengine duniani katika kuadhimisha wiki ya kimataifa ya Vijana ambayo imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka kwa makundi mbalimbali ya vijana na wadau mbalimbali wa masuala ya vijana kukutana katika maeneo tofauti na kuzungumza juu ya mambo tofauti juu ya vijana. Sina uhakika mwaka huu maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika wapi kwani mpaka sasa, wizara inayohusika haijaweka wazi ni wapi jukumu hilo litafanyika. Hata hivyo, hayo hayatanifanya mimi kama mdau na mwanaharakati wa vijana kuacha kutimiza wajibu wangu wa kuwasemea vijana. Kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho hayo inasema, “ONEKANA: SIKIKA, USHIRIKI WA VIJANA KWA MAENDELEO”! Hivyo ni wajibu wetu kama vijana na wanajamii kutafuta namna ya kuwafikia vijana katika siku hii muhimu ya maadhimisho hayo kimataifa.

Mheshimiwa Rais, kwa muda mrefu sasa vijana wa kitanzania wamekuwa wakilalamika juu ya mazingira magumu yanayowakabili katika harakati zao za kimaisha. Hii inatokana na jinsio hali ilivyobadilika tofauti na matarajio waliyokuwa nayo juu yako kabla na baada ya kuchaguliwa kwako kuwa rais wa awamu ya nne wa Tanzania. Hivyo wamekuwa wakijiuliza kama ni kweli kuwa ile kauli ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania” na ile ya “Tanzania yenye neema yawezekana” inawahusu wao au ni kwa wale wachache tu walio katika mazingira ya kujichukulia Chao Mapema. Ninakumbuka wakati unapiga kampeni na kuomba kura kwa watanzania ulikuwa na kauli mbiu nzuri juu ya vijana kuwa utawawezesha Vijana kujiajiri na pia utatoa nafasi za ajira kwa vijana milioni moja kwa mwaka, hivyo kwa miaka mitano ya mwanzo ya serikali yako, zingepatikana nafasi za ajira milioni tano. Kauli mbiu hizo pamoja na nyingine nyingi ndizo zilizokuwezesha wewe kupata ushindi mkubwa uliotingisha na kuuita Ushindi wa Tsunami.

Mheshimiwa Rais, wakati uliporudi jijini Dar es salaam baada ya kuteuliwa Mjini Dodoma kwako kuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi mkuu wa 2005, ulipata mapokezi makubwa sana ambapo pamoja na mambo mengine ulikutana na kilio cha vijana juu ya matatizo mbalimbali yanayowakabili. Hivyo walipoongea nawe katika Ukumbi wa Diamond Jubelee ulisema kuwa umesikia kilio chao na hivyo uliahidi kujitahidi kutafuta namna ya kuwasaidia vijana hao kutoka katika hali ngumu ya maisha inayowakabili. Hata hivyo hali imekuwa ni tofauti na matarajio yao ndani ya miezi kumi na nane tangu serikali yako iingie madarakani. Swali la vijana ni je ulikuwa unawalaghai au kuna vitu ulivyokutana navyo ikulu vikakwamisha dhamira yako njema uliyokuwa nayo dhidi yao? Swali hili limekuwa likiulizwa kwani mambo yanayoendelea kwa vijana baada ya kuingia madarakani serikali yako yamewakatisha tamaa na wengi wamekuwa wakijuta kwani hawakutarajia kuona hayo hasa kwa kuzingatia kuwa eti (ulikuwa mshikaji wao) katika hali ngumu ya maisha. Vijana wamekuwa wakiuliza kuwa je zile ajira milioni moja ulizoahidi kila mwaka bado zipo au zinachukuliwa na wawekezaji wa nje au ni kwa vijana wapi, na kwa wale uliowaahidi kuwawezesha kujiajiri ni hao serikali yao iliyoamua kuwafukuza mjini kwa kuwa wanachafua miji kwa kutembeza bidhaa mikononi na kuuza mitumba katika maeneo ambayo mnadai si maeneo ambayo si rasmi? Je ni wapi mlipowatengea vijana hao penye nafasi na miundo mbinu bora na wakakataa kwenda?

Mheshimiwa Rais, hivi karibuni nilikuwa jijini Dar es salaam, ambapo kwa bahati nzuri nilipata nafasi ya kuzunguka katika maeneo mengi ya jiji hilo, kwa sehemu kuwa vijana waliokuwa wakifanya biahsar zao za kuuza mitumba na bidhaa nyingine (maarufu kama wamachinga), wameondolewa na kupelekwa katika maeneo yasiyo na biashara wala miundo mbinu, matokeo yake wengi wamekata mitaji yao kiasi cha baadhi yao kuamua kujiua baada ya kubomolewa kwa vibanda vyao bila kujua kama huko walipokuwa wanapelekwa ni sehemu sahihi au la. Zoezi hilo limehamia pia kwa wapiga debe na makondakta wasio na shughuli maalum katika vituo mbalimbali vya daladala. Hata hivyo licha ya hatua hiyo kuchukuliwa kwa ajili ya vijana hao ambao nao ni wahitaji na wamekuwa wakitegemea kupata riziki kupitia maeneo hayo, bado hakuna hatua mbadala zimechukuliwa katika kuwasaidia wahusika hao ili wasiende kufanya zile biashara za kutegemea mtaji wa nguvu zao (wizi, ujambazi, umalaya na ukahaba). Zoezi hili si la jijini Dar es salaam tu, bali ni katika maeneo yote ya nchi yetu. Kwa sehemu kubwa inaonekana kuwa tumehamisha tatizo tkutoka sehemu moja na kulipeleka sehemu nyingine, kwani hakuna mbinu mbadala za kuwasaidia hao tuliowaondoa mjini. Mfano ulio hao ni wale wote waliokuwa wakifanya biashara ya ukahaba na uchangudoa pale Manzese, nasikia wamahamishia biashara yao pale Buguruni na wanafanya biashara yao hadharani bila woga wowote.

Mheshimiwa Rais, mwaka jana serikali yako ilitenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa kila mkoa ili kuweza kuwakopesha wajasiriamali wadogo, hata hivyo mpaka sasa ninapokuandikia barua hii, kwa kweli fedha hizo zimeishia mifukoni mwa watu wachache tu tena wale walio na mitaji na fedha, vijana na wananchi wengi wa chini, hakuna hata mmoja aliyepata mikopo hiyo. Sasa tunajiuliza kama ni kweli serikali yako ilikuwa makini juu ya hilo au bado hali ni ile ile ya kuwabeba wale walio nacho na wale wasio nacho hata ile mitaji yao midogo wananyang’anywa kwa kuwabomolea vibanda vyao na kuchukua mitumba yao na vyakula vya akina mama ntilie? Hili unaweza kulithibisha kwa kufanya ziara katika mabenki na vyombo vyote vilivyopewa dhamana ya kutoa mikopo hiyo. Kwa hali hii vijana wanauliza kama kweli wewe ndie waliyekuwa wanakutarajia au bado wamatarajie mwingine ajaye?

Mheshimiwa Rais, pamoja na kauli nzuri za viongozi wetu juu ya kuwataka vijana kurudi vijijini kwa ajili ya kujiingiza katika kilimo na ufugaji lakini ukipita katika maeneo mengi ya vijijini utakutana na hali mbaya ya maisha ya huko na wala hakuna miundo mbinu mizuri wala pembejeo kwa wale wote wanaoamua kujikita katika sekta hizo muhimu. Na kwa wale wachache wanaojifanyia shughuli hizo, bado hawapati soko wala mazao yao hayanunuliwi kwa wakati na kama wanauza mazao yao basi ni kwa wafanyabiashara ambao wananunua mazao hayo kwa bei ya chini na hivyo kuwa ni hasara kwao. Nani atawasaidia hao katika mikakati yao ya kujikwamua kiuchumi? Wakati ninaandika barua hii nikakumbuka juu ya kashfa iliyomkumba mbunge mmoja aliyekopa mabilioni ya fedha katika benki moja kwa dhamana ya serikali huku wajasiriamali wadogo wakikosa fursa hiyo, pia kuna taarifa ya mbunge mwingine aliyekiri kuwa yeye anamiliki benki hapa nchini na huku mbunge mwingine aliyepewa kibali cha kujenga Hoteli ya Kitalii kwenye eneo ambalo haliruhusiwi kwani itaathiri mazingira ya bahari lakini akapewa kibali tu. Hapo pia vijana wanauliza, mbona wao hata kama wamejiunga katika vikundi vya watu wasiopungua hamsini wanawezi kupata mikopo ili nao wafanye biashara zitakazowanyanyua kiuchumi na hivyo kuitwa wajasiriamali wa ndani? Kwa hili unasemaje mheshimiwa rais?

Mheshimiwa Rais, vitendo vya unyanyasaji na kuwaua vijana na wachimbaji wadogo vinavyofanywa na wachimbaji wakubwa ambao wengi si raia katika maeneo mbalimbali ya migodi ya madini yetu ni sehemu ya kilio cha kila mara huku serikali yako ikifumbia macho bila kutoa walao kauli ya kukemea matendo hayo ni sehemu ya swali ambalo vijana wamekuwa wakiuliza. Wao wana nafasi na kauli gani katika kujinufaisha na ujtajiri huo ambao ni sehemu ya neema kubwa Mwenyezi Mungu aliyoitunukia Tanzania na sasa inachukuliwa na wageni kama mali isiyo na wenyewe? Ni vema ukawajibu vijana hata hili.

Mheshimiwa Rais, hivi karibuni ulioongoza watanzania katika kampeni ya upimaji wa hiari wa VVU/UKIMWI. Kimsingi ninakupongeza sana kwa hatua hiyo muhimu uliyoichukua, hasa baada ya kuungwa mkono na baadhi ya wabunge wakiongozwa na Spika wa Bunge, Mhe. Samwel Sitta na Waziri Mkuu, Mhe. Edward Lowassa na wake zao. Hata hivyo bado ni lazima tujiulize kama hatua hii ni ya kitaalamu au ni ya kisiasa zaidi. Pmaoja na hayo ni vema serikali pia ikawa na msaada kwa wale wote walioamua kuwa wazi baada ya kuthibitika kuwa wanaishi na VVU. Nina fahamu juu ya vikundi mbalimbali vya vijana katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu wanaoishi na VVU, lakini pamoja na wao kukaa kama familia, bado hawapati misaada itakayowawezesha walao kuwa na miradi ya kuwapatia mapato ili waweze kujikimu kimaisha kwani iwapo vijana hawa wasipopata misaada hivyo, ni hatari sana kwa maisha ya watanzania wengine kwani wanaweza kuamua kusambaza VVU kwa makusudi bila kujulikana kwani licha ya kuwa wamekuwa wazi kuwa wanaishi na VVU, wengi wao wamekuwa wakitongozwa na wanaume/wanawake wengine kwa kuwa hawajionyeshi na kwa kweli wengi wao ni wazuri wa sura na miili na afya zao ni nzuri na wala huwezi kuwatilia shaka kama hutaelezwa kuwa wanaishi na VVU. Hili pia ni swali la vijana kwako.

Mheshimiwa Rais, nina mengi ya kuzungumza nawe kwa niaba ya vijana wa Tanzania, hata hivyo naomba uniruhusu niseme kuwa umefika wakati wa kuwasiliza vijana, kwani kilio kikubwa cha vijana ni kutokusikilizwa. Hivyo ninakuomba sana ujitahidi pamoja na ratiba yako kutingwa na shughuli nyingi za nchi, utenge walao siku moja ili ukae na vijana wa Tanzania uwasikilize kwani nina imani kuwa wana mambo mengi ya kusema nawe. Ninayasema haya kwa kuwa mpaka sasa hakuna waziri yeyote wa Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana aidha aliyekuwa Waziri Mhe. Prof. Jumanne Maghembe au wa sasa Mhe. John Chiligati au hata manaibu mawaziri wao, aliyewahi kupanga na kukaa na vijana na kuwasikiliza katika kilio chao. Fahamu kuwa kwa sehemu kubwa inawezeakana kuwa mengi huyafahamu na wala hujayasikia yote, lakini ukipata nafasi ya kuwasikiliza vijana utafahamu hayo na mengi zaidi ambayo ulikuwa hujayasikia.

Mheshimiwa Rais, nimalizie kwa kusema kuwa, vijana wanahitaji kusikia jambo jipya, wengi wanatamani kupata nabii mpya wa kuwaokoa na wala habari za kisiasa si za lazima kwao kwani wengi wana maisha magumu, hawajui watakula nini kesho na wala maisha yao watayaboresha vipi. Hivyo unaombwa kubeba wajibu huo kwa nguvu mpya ili vijana wakiri kuwa sasa wameuona ukombozi ulio tayari kwao. Ni matarajio ya vijana kusikia kitu juu ya hayo na mengine mengi ambayo hayajaandikwa hapa.

Mungu Ibariki Tanzania! Mungu wabariki Vijana wa Tanzania!

Mwanaharakati wa Masuala ya Vijana,

Hillary N. Mkony,
S.L.P. 743, Simu: 0754-000215,
Barua pepe: hillarymy@yahoo.com
ARUSHA.

No comments: