Friday, August 24, 2007

HONGERA ASKOFU MALASUSA; VIJANA TUNAKUTARAJIA!

Hivi karibuni Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) lilifanya mkutano wake mkuu ambapo pia lilikuwa na uchaguzi wa Mkuu wa Kanisa hilo, baada ya aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo Askofu Dk. Samson Mushemba toka mwaka 1992 kumaliza muda wake. Katika mkutano huo, alichaguliwa Askofu Alex Gehazi Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani yenye makao yake makuu Dar es salaam kuwa mkuu mpya wa Kanisa hilo kubwa hapa nchini baada ya Kanisa Katoliki. Kanisa hilo lina idadi ya Dayosisi ishirini hapa nchini na pia maeneo ya Misioni katika baadhi ya Mikoa na nchi jirani.

Kwanza sina budi kumshukuru sana Mungu kwa jinsi alivyoweka mkono wake katika mkutano huo mpaka wakampata mkuu mpya wa Kanisa hilo kwa amani, hasa kwa kuzingatia kuwa mwaka jana zoezi la kumpata mkuu huyo lilisshindikana kiasi cha kusababisha mchakato kuahirishwa kwa muda wa mwaka mmoja. Pili ninapenda kumpongeza sana Baba Askofu Malasusa kwa wajibu huo mzito aliokabidhiwa huku akiwa ni Askofu kijana kuliko maaskofu wengine ambao wamemzidi umri na hata elimu kwani wengine wana shahada ya Udaktari wa Falsafa (Phd) katika Theolojia. Mungu akuwezeshe kusimama imara katika wajibu wako huo ambao ni mzito lakini ni kwa msaada wake tu utauweza.

Pamoja na pongezi zangu hizo kwa Baba Askofu Malasusa, kimsingi nina mambo machache ya kumwelekeza kama changamoto kubwa katika wajibu wake ndani ya Kanisa hilo. Changamoto yangu ni juu ya hali ya vijana ndani ya taifa, jamii na madhehebu ya dini pia.

Kimsingi Baba Askofu Malasusa umechaguliwa kuwa kiongozi mkuu katika kipindi ambacho ni kigumu kiasi hasa kwa upande wa maisha ya vijana. Hii ni kutokana na kuwa vijana wa sasa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimaisha, ikiwemo suala la Utandawazi, ukosefu wa ajira katika sekta iliyo rasmi, mfumo wa elimu duni, hali ngumu ya maisha, mazingira magumu ya ufanyaji wa biashara, ukosefu wa mitaji na urasimu wa upatikanaji wa mitaji na mikopo ya kufanyia biashara, tatizo la matumizi ya dawa za kulevya, kasi ya maambukizo ya VVU/UKIMWI, na sualala mmomonyoko wa maadili ya vijana wetu. Nimependa kuzungumzia mambo haya kwa kuwa wewe kama kiongozi wa dini na mwenye wajibu wa kuwaongoza waumini wako katika hali ya kumfahamu na kumwishia Mungu, hata hivyo vijana ambao wanaishi katika mazingira haya magumu ya kimaisha, wanashindwa kusimama imara katika nafasi zao za kutumika katika madhehebu yetu ya kidini.

Hivyo ni wajibu wa wanajamii wote kuoni kwa namna gani wanaweza kushiriki katika wajibu wa kuwasaidia vijana ili waweze kusimama katika zamu zao kimaisha. Ninayasema haya kwa uchungu kwa kuwa nimeona kwa sehemu kubwa jinsi ambavyo vijana wamekuwa wakidharauliwa na kubezwa katika nafasi zao na hivyo kuonekana kuwa kama kitu kisicho na thamani yoyote kijamii. Vijana wamekata tamaa na kupoteza tumaini la maisha na ndio maana kila mara pamoja na mahubiri mazuri yanayotolewa katika nyumba zetu za ibada, badop vijana wetu wanaendelea kutenda maasi na mambo machafu na ya kutisha. Hata hivyo inawezekana kuwa viongozi wetu wa dini hamjafahamu ni nini kinahitajika kufanywa kwa vijana hao ili tuweze kuwaokoa katiak maangamizo makubwa yanayowakabili.Katika hilo ni lazima sote tujiulize sasa ni wajibu wa nani kufanya kitu kwa ajili ya maisha na malezi ya vijana.

Kama vile Katiba ya nchi yetu inavyoonyesha ni kuwa kuna mihimili mitatu inayoshirikiana katika utendaji wa kazi hapa nchini, mihimi hiyo ni Serikali, Bunge na Mahakama. Vivyo hivyo katika malezi ya vijana kuna mihimili mitatu inayopaswa kufanya kazi kwa pamoja. Mihimili hiyo ni Serikali, Jamii (Wazazi, walezi, waalimu n.k.) na Taasisi za dini. Mihimili yote hii inapofanya kazi yake inavyopasa, ndipo tutakapoona utendaji mzuri na wenye kuleta tija katika maisha ya vijana.

Sina uhakika kama ni viongozi wangapi wa kidini leo wanaofahamu juu ya hilo, lakini ni nafasi yangu hii naomba kuitumia kupitia kwako leo, kuwafikishia viongozi wengine ujumbe kutoka kwa vijana kuwa, sasa umefika wakati wa kuwafikia vijana. Hii ni kwa kuwa, vijana wamekuwa wakiumia, lakini hakuna wa kuwasaidia. Pamoja na kuwa kuna wajibu wa kiserikali, na wa kijamii, lakini nadhani makundi hayo mawili yamepoteza mwelekeo na hivyo hawajui ni nini wanaweza kufanya tena kwa ajili ya maisha ya vijana. Kwa kuwa hayo yameshindikana kwao, basi ni wajibu wenu kama walezi wetu wa kiroho, kuubeba wajibu huu ili kuokoa kizazi hiki kilichoharibika, ambacho Biblia inakiita kizazi cha nyoka. Ni vema madhehebu yote ya dini yakafahamu kuwa suala la kuwapatia vijana wetu ajira ni letu sote, suala la kuwapatia elimu vijana wetu ni letu sote, suala la kuwalea vijana katika maadili ya kitanzania ni letu sote, suala la kukemea kasi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana ni letu sote, suala la kusaidia kuondoa kasi ya maambukizi ya VVU/UKIMWI ni letu sote. Hivyo hakuna ambaye atakwepa kubeba lawama kwa lolote litakalomtokea kijana wa leo wakati tuna nafasi ya kukemea, kuonya na kushauri hata kwa fimbo ikibidi.

Ni kweli kuwa Baba Askofu Malasusa umepewa wajibu huo ukiwa kijana mwenye nguvu, na Biblia inawasifu na kuwapongeza Vijana kuwa, “NIMEWAANDIKIA NINYI VIJANA, KWA KUWA MNA NGUVU NA NENO LA MUNGU LINAKAA NDANI YENU, NANYI MMEMSHINDA YULE MWOVU”! 1 Yohana 2:14b, hivyo hebu onyesha nguvu za ujana wako ili uweze kuwasaidia vijana hao waliopoteza matumaini yao chini ya jua hili. Huu ni wajibu mzito uliokabidhiwa, lakini Mungu mwenyewe ataenda kukuongoza na kukupigania katika wajibu huu.

Nimalizie kwa Neno linalosema kuwa, “EE BWANA, NIMESIKIA HABARI ZAKO NAMI NAOGOPA, EE BWANA FUFUA KAZI YAKO KATIKATI YA MIAKA. KATIKATI YA MIAKA TANGAZA HABARI YAKE. KATIKA GHADHABU KUMBUKA REHEMA”! Habakuki 3:2.

Mungu akuwezeshe ili uweze kusimamia ufufuo mpya wa kazi ya kuwalea Vijana ndani ya nje ya Taifa letu la Tanzania. Sisi pia tupo nyuma yako tukikuombea na kukutia moyo. Kuna mengi ya kukueleza Baba Askofu, lakini itoshe tu kwa mwanzo huu kusema kuwa mengine tutakueleza tukipata nafasi kwa kadri Mungu atakavyotujalia.

“Inuka! Maana shughuli hii yakuhusu wewe; na sisi tupo pamoja nawe. Uwe na moyo Mkuu! Ukaitende”! – Ezra 4:10.
Mungu Ibariki Tanzania! Mungu wabariki Vijana wa Tanzania!

Mwanaharakati wa masuala ya Vijana,

Hillary N. Mkony,
S.L.P. 743, Simu: 0754 – 000 215,
Barua pepe: hillarymy@yahoo.com
ARUSHA.

No comments: