Friday, August 24, 2007

HONGERA KABWE: WEWE NI SHUJAA WA VIJANA!

Kwanza ninapenda kuwashukuru sana wasomaji wangu ambao walinipigia simu na wengine kunitumia ujumbe mfupi wa simu (sms), kunipongeza kwa makala yangu ya wiki iliyopita iliyokuwa na ujumbe kwa Rais Kikwete, iliyokuwa na kichwa, “Mhe. Kikwete Vijana wanasema hivi …….”! Kimsingi ninashukuru sana wote kwaniwalinipa moyo na changamoto kubwa kwangu juu ya wajibu wangu wa kuwasemea vijana. Ahsanteni sana na ninaomba mzidi kunishauri kila mara.

Wiki iliyopita, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilimsimamisha kuhudhuria vikao vya mikutano miwili ya bunge hilo, Mhe. Zitto Zubeir Kabwe kwa madai ya kusema uongo bungeni. Katika hatua hiyo ambayo imepokelewa kwa mitazamo tofauti na wananchi, wanajamii, wanasheria, wasomi na wanaharakati mbalimbali hapa nchini. Kimsingi kulikuwa kunahitajika mafafanuzi ya hali juu kutokana na hatua hiyo ambayo imeonekana kuwa bunge hilo limetumika kama chambo katika kuminya demokrasia badala ya kuijenga na kuitetea. Kwa sehemu kubwa kumekuwa na kauli kutoka kwa watu mbalimbali juu ya hatua hiyo ya kusimamishwa kwa Mhe. Kabwe. Hata hivyo nami kama mmoja wa wadau wa vijana na mwanaharakati, nitapenda kuongelea jambo kwa sehemu tu juu ya suala hilo. Hata hivyo mimi nitapenda kuliongelea suala hilo kwa mtazamo wa tofauti hasa kwa kuzingatia kuwa Zitto ni sehemu ya vijana na kwa hivyo jambo analolifanya kama mbunge, pia linawagusa vijana ambao yeye ni mwakilishi wao katika chombo hicho cha kutunga sheria. Hivyo nitapenda kuzungumzia juu ya nafasi na wajibu ambao umeendwa kuonyeshwa na mbunge huyo kijana ambaye bado ana nafasi kubwa ya kuwatumikia wapiga kura wake na watanzania kwa ujumla.

Kwa sehemu kubwa sisi kama wapiga kura wa Tanzania tunafahamu kuwa tuna wabunge wetu wanaotuwakilisha katika chombo hicho cha kutunga sheria, hata hivyo kwa sehemu kubwa tumekuwa tukishuhudia juu ya wengi wa wawakilishi wetu hao kushindwa kutumia nafasi na wajibu tuliyowapa kama wapiga kura wao na badala yake kubaki wakishabikia masuala ya vyama vyao bungeni. Kwa hali hii ndipo sisi kama wapiga kura tumekuwa tukijiuliza, ndicho tulichowatuma muende mkafanye bungeni? Mbona kuna mambo mengi ambayo ni ya msingi na yanahitaji kuzungumzwa na wabunge wetu na hivyo kupatiwa majibu toka serikalini. Sasa waheshimiwa mnapoacha kutekeleza wajibu huo ulio muhimu kwenu na kuamua kuwa wajibu hoja kwa niaba ya serikali, kwa hali hiyo mwataka tuwaeleweje? Ni vema mkafahamu kuwa mmepewa wajibu wa kuwakilisha hoja na haja za wapiga kura wenu serikalini kupitia katika bunge.

Mara kwa mara nimekuwa nikifuatilia na kutazama juu ya nafasi za vijana katika wajibu wa kuwatumikia wananchi hapa nchini na pengine duniani. Kimsingi nimesoma katika historia juu ya vijana wengi ambao walikubali kuwa wawakilishi wa watu na hata wengine kufikia mahali pa kukubali kutoa kafara maisha yao. Miongoni mwao ni pamoja Mwanaharakati wa ukombozi Afrika Kusini marehemu Steve Biko ambaye aliuwawa na makaburu akiwa na miaka 30. Wengine ni pamoja Yesu Kristo ambaye alimua kuyatoa maisha yake kwa ajili ya wanadamu wote na hatimaye kuuwawa kwa kuangikwa msalabani akiwa na miaka 33. Pia katika msahafu wa Kikristo (Biblia), tunasoma juu ya kijana mwingine ambaye aliweza kulinda na kutetea nafasi yake kama kijana ndani ya jamii, kijana aliitwa Yusufu, ambaye aliukuwa ni mtumishi katika jumba la Kiongozi wa jeshi la Kimisri ambaye alikuwa anaitwa Potifa. Mke wa Potifa alikuwa anamtaka Yusufu ili aweze kufanya naye ngono, lakini yeye (Yusufu) alikataa na kuamua kukimbia na hata kumuachia nguo yake, jambo hili lilikuwa ni gumu kwani lilimgharimu Yusufu kiasi cha kufungwa gerezani. Lakini aliilinda heshima na hadhi yake na pia kumheshimu Mungu wake. Hawa ni sehemu tu ya mifano ya watu ambao walikuwa ni vijana lakini walikuwa tayari kupoteza maisha yao kwa ajili ya wengi. Nimeona niitumie mifano hii kwa kuonyesha jinsi ambavyo Mhe. Zitto Kabwe alivyokubali kutumia nafasi yake kama kijana na mwakilishi wetu kutetea maisha na uchumi wa watanzania. Ninakiri kuwa katika mazingira ya sasa ni watu wachache sana ambao wana roho na moyo kama wa Kabwe. Hii ni kwa kuwa wakati wa kchukua hatua za kumuadhibu bungeni, pamoja na kupewa nafasi na kutakiwa kujitetea yeye aliishia kwa kusema kuwa, yeye ni mwanademokrasia, hivyo yupo tayari kwa lolote.

Kwa tukio hili la Mhe. Kabwe linaonyesha jinsi yeye kama mwakilishi wa wapiga kura na kama kijana alivyo na uchungu na upendo kwa nchi yake Tanzania. Hivyo hakuona shida kukubali kusimamishwa kujihusisha na shughuli za bunge huku akipokea nusu mshahara kwa kipindi cha miezi mitano. Naomba ieleweke wazi kuwa, iwapo tungekuwa na wabunge wengi wenye moyo kama wa Mhe. Kabwe, basi kwa sehemu kubwa nchi yetu ingekuwa imetoka kwenye matatizo magumu yaliyopo. Yapo mambo mengi yanayotokea, ambayo yamekuwa ni matatizo makubwa kwa wananchi na vijana wa Tanzania, lakini ni nani anaweza kuyawakisilisha mbele ya serikali au hata kukemea, inaonekana hakuna, wengi wapo kwa ajili ya maslahi yao tu. Mara kwa mara nimekuwa nikijiuliza bila kupata majibu, kuna ni nani nabii mpya wa Tanzania, mbona wale tuliokuwa tunawatarajia ndio hao wametutosa na kutuacha kwenye mataa, hatujui ni wapi pa kukimbilia kwani kote huko kumekuwa ni pabaya zaidi ya matarajio yetu. Hapo ndipo ninaposhindwa kuelewa kama kweli waliopo madarakani sasa ni wale tuliokuwa tunawatarajia au kuna wengine tuwasubiri.

Mambo mengi yanawakabili watanzania na hususan vijana, lakini wale ambao leo ndio tunawaita waheshimiwa wawakilishi wetu, wamekaa kimya kama vile mambo hayo hayawahusu, wamekuwa tayari kuacha sisi tufe ili mradi wao wanapokea maslahi yao makubwa kila iitwapo leo. Tazama jinsi tatizo la dawa za kulevya linavyowaangamiza vijana, tazama kasi ya maambukizo ya VVU/UKIMWI ilivyo hapa nchini, tazama suala umasikini unavyowakabili watanzania wengi, tazama hali ya ukosefu wa ajira, elimu nzuri na hata fursa nzuri za kufanya biashara hakuna, tatizo la ukosefu wa mitaji au hata mikopo ni kubwa kwa jamii, yote haya ni sehemu ya mambo yanayowakabili watanzania, lakini hakuna anayeyaona, wote wapo kwa ajili ya maslahi yao. Kwa hali hii tunao wawakilishi kweli?

Kinachoonekana katika suala hili la Mhe. Kabwe pamoja na mambo mengi yanayotokea katika bunge letu hili ambalo kinara wake aliahidi kuliongoza kwa VIWANGO NA KASI, ni katika hali ya kulinda maslahi ya Chama, wawakilishi wetu wengi hawana uchungu na maslahi ya taifa letu la Tanzania, bali wana maslahi na matumbo yao na Vyama vyao tu. Naomba ieleweke kuwa kama kweli Bunge letu na waheshimiwa wabunge wangekuwa na maslahi na Tanzania, wangemsikiliza mbunge mwenzao na kuipitisha hoja yake ili kuweza kumchunguza Mhe. Waziri Karamagi, lakini kwa kuwa hawana maslahi na Tanzania ndio maana waliamua kumsulubu mwenzao Kabwe. Hapo ndipo ninapojiuliza, ni lini watakapopatikana wawakilishi wenye uchungu na maslahi na Tanzania.

Nimalizie kwa kumtia moyo Mhe. Kabwe kuwa yeye ni sehemu tu ya watu walioonyesha hali ya kuthubutu kusema, jambo uthubutu wake umemgharimu, lakini afahamu kuwa hiyo ni gharama ya kuwa MKWELI. Kama alivyosema Mwanafalsafa Steve Biko kuwa “HERI KUFA UKIWA NA KAULI INAYOISHI, KULIKO KUISHI UKIWA HUNA KAULI”! Hivyo Mhe. Kabwe usikate tamaa, tumekuona ukweli wako na ulivyokugharimu, tumefahamu kuwa u shujaa wetu sisi Vijana, wewe songa mbele na sisi TUPO NYUMA YAKO, tunakufuata. Umetuonyesha mwanga mpya vijana na hivyo tuna wajibu wa kuufuata, usikatishwe tamaa na hayo, wewe ni kamanda, nyuma yako lipo jeshi kubwa la Vijana, Tunasubiri kauli yako.

Mungu Ibariki Tanzania! Mungu Wabariki Vijana wa Tanzania!

Mwanaharakati wa Masuala ya Vijana,

Hillary N. Mkony,
S.L.P. 743, Simu: 0754-000215,
Barua pepe: hillarymy@yahoo.com
ARUSHA.

No comments: